Shabaha yangu ya kuendelea na masomo ilifika tamati. Kwa kuwa huwezi kutazamia tasa kuzaa au kuku kuyatoa maziwa, haya yalikuwa sawia nami kufikiri kuyaendeleza masomo yangu ilhali sikuwa na yeyote wa kunidhamini.
Maisha yangu yalikuwa ni kama yamewekewa alama ya kudonesha kwani niliyapenda masomo kupindukia. Nilichobakia nacho tu ni nguvu za kusadiki na kumpeperushia Mola sala zangu nyenyekevu nikitumai kwamba atanipa jawabu.
Maisha Ni Moshi
Kiswahili Kitukuzwe.
Tuesday, March 13, 2012
Thursday, February 9, 2012
Kisa 3: Matukio ya Mtihani wa Mwisho wa Msingi
Matokeo ya mitihani ile yalipotangazwa moja kwa moja hewani, nilikuwa katika safu ya watahiniwa wachache waliokwagura alama takriban zote. Mtima wangu ulibopabopa kwa kiwewe cha bashasha bin liwazo kwani nilijua wazi kama mchana kuwa nyanyangu ataniezeka mkate mzima wa boflo. Boflo kijijini chetu ilikuwa nadra kama maji kwenye jangwa la Sahara na nilijua kuwa vijana majirani watataka kusherehekea na mimi pia ijapokuwa sherehe yao itakuwa ya boflo tu.Waliosema zawadi ni mbolea ya urafiki hawakupotoka hata kidogo.
Kisa 2: Joka Jeusi
Nilikuwa nimebarizi chini ya kivuli cha mti wa mkakasi upepo mwanana ukivuma. Nilikuwa mwindaji gwiji aliyejulikana kotekote vijijini kama ada. Ghafla kama kifo, joka jeusi tititi lilinirukia kwenye kichwa na kunidona. Kasi na uzito wa joka lile zilinizaba chini na kunitoa fahamu kwa muda usiozidia sekunde moja. Katika hali ile, ukelele nilioutoa ulitosha kumfanya bubu asikie tena. Hofu na maumivu yalinizidi unga na miguu yangu ilianza kupiga mateke hewani. Povu zilinitoka mdomoni kwa fujo. Nilichungulia kaburi kwa macho yote mawili na nilijua roho yangu haingekuwa na dakika nyingi kuishi duniani humu kamwe. Nilisema ombi fupi nikatubu dhambi zangu na niliamini eti Mola aliliskia sala hilo. Niliyafunga macho yangu na kukikaribisha kifo kije kiniteke nyara na kuniondolea uchungu ule. Mui hawi mwema. Siku yangu ilishawadia na sikuwa na nguvu ya kusema la. Liwalo na liwe.
Tuesday, December 27, 2011
Kisa 1
Bila kubananga wakaa, ningependa kuwajulisha hili kwa muda mfupi uliosalia.
Palitukia banati mmoja katika kijiji chetu Kanyageni na mwili wake ulikuwa umelainika kama parachichi bivu. Maziwa yake yalisimama tisti boriti kifuani mwake. Mashavu yake yalijaajaa na yaliunda vidumbwi maridadi kila alipocheka. Maninga yake yalikuwa ya kikombe. Mdomo wake wa chini uliokuwa mkubwa kidogo kuliko wa juu uliyafanya meno yake yaonekane wazi kila alipoangua kicheko. Meno yake yalingaaa utadhani saluji.Vijana wengi walimtamania na vijana wengi walijaribu bahati yao.
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuzama shimoni lile, jambo ambalo, kuzingatia utamaduni lilikuwa mwiko. Maziwa yalishaamwagika. Niliapa kutorudia jambo lile tena kwani maisha yangu yalishaakosa maana kwangu yakawa sampuli ya tupu la yai.
Nilikuwa nishaambukizwa ugonjwa mbaya wa ukimwi.
Palitukia banati mmoja katika kijiji chetu Kanyageni na mwili wake ulikuwa umelainika kama parachichi bivu. Maziwa yake yalisimama tisti boriti kifuani mwake. Mashavu yake yalijaajaa na yaliunda vidumbwi maridadi kila alipocheka. Maninga yake yalikuwa ya kikombe. Mdomo wake wa chini uliokuwa mkubwa kidogo kuliko wa juu uliyafanya meno yake yaonekane wazi kila alipoangua kicheko. Meno yake yalingaaa utadhani saluji.Vijana wengi walimtamania na vijana wengi walijaribu bahati yao.
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuzama shimoni lile, jambo ambalo, kuzingatia utamaduni lilikuwa mwiko. Maziwa yalishaamwagika. Niliapa kutorudia jambo lile tena kwani maisha yangu yalishaakosa maana kwangu yakawa sampuli ya tupu la yai.
Nilikuwa nishaambukizwa ugonjwa mbaya wa ukimwi.
Saturday, September 11, 2010
Uzuri Wa Mkakasi...
Mbona kilio mwanangu nakuuliza nambie? Ukilia unavyofanya nani atanipanguza mimi yanayonitiririka rohoni mwangu? Maisha yana majaribu yake lakini mbona kukinai matumaini? Mambo huenda yakaenda sege mnege moja baada ya mengine utadhani umerogwa. Marafiki huenda wakahepa ukabaki hauna yeyote kukuondolea upweke. Marafiki hawa hawakuwepo ulipozaliwa kwa hivyo mbona uukubalishe moyo wako kuweweseka na dhana hiyo? Usidhoofike mwanangu, sitakwacha mie niliyekuleta humu duniani, Sharti. Nitasimama nawe hadi nisiweze kufanya hivyo tena, mwanangu. yavute machozi yako mwanangu. Tafadhali nisikize unirejeshee raha moyoni mwangu mwanangu. Sijapata kuondoka ninapoketi kwa siku mbili nikikutizama wewe mwanangu. Ongea uniambie lolote angalau mwanangu. Usilie tena mwanangu ukilia utaniletea maradhi pia. Maradhi ya moyo. Mungu nimemwomba, nikamwomba na nikamwomba tena lakini yaonekana inabidi nisali tena na tena. Tafadhali koma kilio mwanangu, Mumbu husaidia anayetamania kusaidiwa. Nitaimba wimbo huu hadi sauti inipotee Sharti mwanangu.
Tuesday, July 13, 2010
Dibaji
Ninaandika visa hivi nikiwa na lengo moja hususan. Kuandika kwa minajili ya kuwavutia watu wowote wale wanaoienzi lugha hii mufti ya Kiswahili. Kiswahili nakienzi kwa mvuto usioweza kumithilishwa na lugha yeyote ile. Kiswahili utamu wake umezidi utamu wowote ule ambao umewahi pitia kwenye ulimi wangu.
Kiswahili kitukuzwe.
Kiswahili kitukuzwe.
Subscribe to:
Comments (Atom)