Thursday, February 9, 2012

Kisa 3: Matukio ya Mtihani wa Mwisho wa Msingi

Matokeo ya mitihani ile yalipotangazwa moja kwa moja hewani, nilikuwa katika safu ya watahiniwa wachache waliokwagura alama takriban zote. Mtima wangu ulibopabopa kwa kiwewe cha bashasha bin liwazo kwani nilijua wazi kama mchana kuwa nyanyangu ataniezeka mkate mzima wa boflo. Boflo kijijini chetu ilikuwa nadra kama maji kwenye jangwa la Sahara na nilijua kuwa vijana majirani watataka kusherehekea na mimi pia ijapokuwa sherehe yao itakuwa ya boflo tu.Waliosema zawadi ni mbolea ya urafiki hawakupotoka hata kidogo.

Kisa 2: Joka Jeusi

Nilikuwa nimebarizi chini ya kivuli cha mti wa mkakasi upepo mwanana ukivuma. Nilikuwa mwindaji gwiji aliyejulikana kotekote vijijini kama ada. Ghafla kama kifo, joka jeusi tititi lilinirukia kwenye kichwa na kunidona. Kasi na uzito wa joka lile zilinizaba chini na kunitoa fahamu kwa muda usiozidia sekunde moja. Katika hali ile, ukelele nilioutoa ulitosha kumfanya bubu asikie tena. Hofu na maumivu yalinizidi unga na miguu yangu ilianza kupiga mateke hewani. Povu zilinitoka mdomoni kwa fujo. Nilichungulia kaburi kwa macho yote mawili na nilijua roho yangu haingekuwa na dakika nyingi kuishi duniani humu kamwe. Nilisema ombi fupi nikatubu dhambi zangu na niliamini eti Mola aliliskia sala hilo. Niliyafunga macho yangu na kukikaribisha kifo kije kiniteke nyara na kuniondolea uchungu ule. Mui hawi mwema. Siku yangu ilishawadia na sikuwa na nguvu ya kusema la. Liwalo na liwe.